Language

Wednesday 6 March 2013

HABARI ZA UCHAGUZI KENYA: MATOKEO KUCHELEWA KUTOKA BAADA YA MITAMBO YA KUHESABIA KUHARIBIKA

Mtandao wa elektroniki wa uwasilishaji na utangazaji wa matokeo ya kura za wagombea urais Kenya umeshindwa kufanya kazi juzi na jana na kuzusha wasiwasi miongoni mwa wananchi.

Mtandao huo ulianza kusuasua tangu juzi mchana na hadi jana mchana ni kura chache tu zilizokuwa zimeongezeka, huku Uhuru Kenyatta wa Jubilee akiendelea kuongoza kwa asilimia 53 dhidi ya Raila Odinga aliyekuwa na asilimia 42 ya kura halali.

Hali hiyo imezua hofu miongoni mwa wananchi, wengi wakianza kuhoji iweje matokeo hayo yacheleweshwe ilhali  Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ilikuwa imeahidi kuwa yangetolewa ndani ya saa 48 baada ya vituo kufungwa Jumatatu.
Mwenyekiti wa IEBC alisema mfumo huo wa kielektroniki umekwama na kwamba hadi jana walikuwa wanahesabu kwa njia ya kawaida baada ya wasimamizi wa uchaguzi kurejea Nairobi kutoka mikoani.
Pia tume hiyo ilikuwa na mpango wa kuingiza kura zilizoharibika kwenye hesabu ya asilimia za wagombea kadri sheria inavyotaka kwa kuwa nazo ni kura zilizopigwa, hatua ambayo inaelezwa itaathiri matokeo na kusababisha uchaguzi wa marudio.
Katika matokeo ya awali yaliyokwishatangazwa, kura 320, 000 zilizoharibika hazikuwa zinajumlishwa.
Hatua hiyo imewagawa wagombea hao wawili wanaochuana vikali, Uhuru na Odinga. Wakati uongozi wa Muungano wa Cord umeitaka IEBC kuacha kuonyesha matokeo ambayo hayahusishi kura zilizoharibika, Mgombea Mwenza wa Uhuru, William Ruto alipinga kitendo hicho, akisema tume ilikuwa inataka kuvuruga uchaguzi.
Vyama vyote viwili, Jubilee na Cord viliwataka mashabiki wake kuwa watulivu kusubiri matokeo hayo.

Vigogo waanguka ubunge

Katika matokeo ya ubunge, baadhi ya wanasiasa maarufu, wakiwamo mawaziri, naibu mawaziri na waliokuwa wabunge wameanguka vibaya.
Mawaziri walioanguka ni Henry Kosgey wa Maendeleo ya Viwanda, Sally Kosgei (Kilimo), Charity Ngilu (Maji) na Amos Kimunya (Usafirishaji).
Naibu Mawaziri walioangushwa ni Ndiritu Mureithi, Mwangi Kiunjuri, mbunge wa zamani wa Naivasha, John Mututho na Kiema Kilonzo aliyekuwa anagombea ugavana wa Kitui.
Kosgey ambaye pia ni Mwenyekiti wa ODM alianguka katika nafasi ya useneta baada ya kiti hicho kunyakuliwa na Stephen Sang wa United Republican Party (URP).

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...