Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imesogeza mbele tarehe ya
usikilizwaji wa maombi ya dhamana ya msanii wa fani ya maigizo,
Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu, anayekabiliwa na kesi ya kuua bila
kukusudia.
Lulu aliwasilisha mahakamani hapo maombi ya dhamana, kupitia kwa jopo la mawakili wake linaloongozwa na Wakili Kennedy Fungamtama, Makamu wa
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Peter Kibatala na Fulgence Masawe wa Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Maombi hayo yalikuwa yamepangwa kusikilizwa leo na Jaji Zainabu Mruke, lakini yamesogezwa mbele hadi Jumatatu, Januari 28, 2013.
Hata hivyo taarifa ya Mahakama (notice) ya
kusogezwa mbele kwa usikilizwaji wa maombi hayo, kwenda kwa mawakili wa
pande zote haikueleza sababu, lakini pengine hiyo ni kwa sababu leo ni
Sikukuu ya Maulid.
Lulu anakabiliwa na mashtaka ya kumuua bila
kukusudia aliyekuwa msanii maarufu wa fani hiyo nchini, Steven Kanumba,
kinyume cha kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu.
Awali kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kukamilisha hatua za awali ukiwamo
upelelezi, huku akikabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia kinyume cha
kifungu cha 196.
Hata hivyo, baada ya kukamilika kwa upelelezi,
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alimbadilishia mashtaka na kuwa ya kuua
bila kukusudia, na Desemba 21, 2012, alisomewa maelezo ya kesi yakiwamo
maelezo ya mashahidi watakaotoa ushahidi.
Baada ya kusomewa maelezo hayo, kesi hiyo
ilihamishiwa Mahakama Kuu ambayo ndio ina uwezo wa kusikiliza mashtaka
yanayomkabili. Tayari kesi hiyo imeshasajiliwa Mahakama Kuu kuwa shauri
la jinai la kuua bila kukusudia, lenye namba ya usajili 125 la mwaka
2012.
Kutokana na mabadiliko hayo ya mashtaka, sasa
mshtakiwa kupitia kwa mawakili wake hao, amewasilisha maombi ya dhamana
chini ya hati ya dharura wakiomba yasikilizwe na kuamuriwa mapema kwa
madai kuwa mshtakiwa amekaa rumande kwa muda wa miezi saba na kwamba
kosa lake linadhaminika.
Kwa mujibu wa hati ya maombi iliyoambatanishwa
na hati ya kiapo cha wakili Kibatala kwa niaba ya mshtakiwa huyo,
wanaiomba mahakama iamuru mshtakiwa apewe dhamana, akiwa au bila kuwa na
wadhamini, au kwa amri na masharti mengineyo ambayo mahakama itaona
yanafaa.
Hati hiyo ya maombi ya dhamana inasema,
“Kwamba tunaomba Mahakama hii Tukufu impe dhamana mshtakiwa akiwa na au
bila kuwa na wadhamini, wakati akisubiri usikilizwaji na uamuzi wa kesi
yake ya msingi, shauri la jinai namba 125 la 2012, iliyoko katika
mahakama hii tukufu.”
No comments:
Post a Comment