Language

Saturday, 16 March 2013

HABARI MUHIMU: VYETI VYA WALIMU KUCHUNGUZWA KWA KINA

Wadau wa elimu Halmashauri ya Wilaya ya Bunda,  mkoani Mara, wameshauri Serikali kufanya ukaguzi wa kina wa vyeti vya taaluma za walimu, ili kubaini kama wanaovitumia ndiyo wamiliki wake halisi. 

Hatua hiyo  inatokana na vyeti hivyo kuonyesha ufaulu mzuri kwa baadhi ya walimu wilayani hapa, lakini hawana uwezo wa kufundisha darasani.
Wakichangia maoni kwenye mkutano wa kujadili maendeleo ya elimu wilayani hapa uliofanyika juzi, wadau hao walisema hali hiyo inaifanya shule kuwa na idadi kubwa ya walimu, lakini  hawana taaluma ya ualimu.
Walisema kwamba hali hiyo ndicho chanzo cha  kushusha kwa taaluma shule za msingi na sekondari.

Hata hivyo, Mkuu wa Sekondari ya Sazira, Mwalimu Josephat Petro alitilia mashaka kama serikali itaweza kuwabana walimu wa aina hiyo kwa sababu wengi wao hujiita watoto wa vigogo.
Mwalimu Petro alisema kutokana na hali hiyo, walimu hao hawaguswi na kuomba Serikali iondokane na tabia ya kulindana ili kunusuru elimu nchini.
“Unakuta vyeti vyao vinaonyesha ufaulu mzuri. Mfano nilikutana na mmoja vyeti vyake vikionyesha kuwa amefaulu vizuri somo la Kiingereza,” alisema Mwalimu Petro na kuhoji:
“Lakini alipopangiwa kulifundisha aligoma kwamba hajui somo hilo, ukimfuatilia unaletewa kimemo cha kukuonya, sasa hii itaipeleka wapi elimu ya Tanzania?”.
Licha ya suala hilo, wadau waliomba Serikali kutatua kwa wakati changamoto zinazoikabili sekta ya elimu nchini, ikiwamo madai mbalimbali ya walimu, uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia hasa vya  maabara  na kuboresha miuondombinu kama  majengo na vyoo.
Awali, Ofisa Elimu Wilaya ya Bunda, William Mabanga alisema lengo la mkutano huo ni kujadili jinsi ya kuinua elimu kwa kuangalia changamoto zinazoikabili  na kuweka mikakati.
Mabanga alisema mikakati itakayowekwa itasaidia kuboresha kiwango cha taaluma kwa shule za msingi na sekondari wilayani hapa.
Mkutano huo ambao ni wa kwanza kufanyika, ulishirikisha wadau 130 kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ambao ni wakuu wa shule za msingi na sekondari, viongozi wa vyama vya siasa na madhehebu ya dini, wamiliki wa shule binafsi na wanaharakati mbalimbali wa masuala ya elimu.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...