Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka amesema mwezi ujao wanatarajia
kutangaza kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta zote.
Akizungumza jana wakati wa mkutano kuhusu sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa
Baraza Kuu la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), alisema kwa muda
mrefu kiwango cha kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta zote
kilikuwa hakijabadilishwa.
“Kwa muda mrefu tulikuwa hatujatangaza kima cha chini cha mshahara,
lakini nafurahi kuwajulisha tu kwamba mwezi ujao tutatangaza rasmi,”alisema
Kabaka.
Pia alitahadharisha kuhusu utitiri wa vyama katika sehemu moja ya kazi
kushauri waajiri wasiruhusu wafanyakazi waanzishe kwa sababu vitakosa nguvu ya
kujadiliana na mwajiri katika kufunga mikataba ya hiyari .
Waziri huyo alisema sekta ya hifadhi ya jamii ina idadi ndogo ya
wanachama waliojiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ukilinganisha na idadi ya
nguvu kazi iliyopo ambayo ni milioni 22.
Awali Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii,
Irene Isaka alisema hadi sasa michango katika mifuko hiyo imefikia Sh 1.4
trilioni na kwamba mafao yanayolipwa yamepanda kutoka Sh500 bilioni hadi
kufikia Sh 724 bilioni.
No comments:
Post a Comment