Mji wa Geita na maeneo ya jirani juzi ulikumbwa na taharuki ya aina yake,
pale mwanamke ambaye anadaiwa kwamba alifariki miaka mitano iliyopita alipoonekana
akiwa hai katika eneo la Kasamwa.
Inadaiwa kwamba Flora Onesmo (45) alifariki Februari 28, 2008 katika
Hospitali ya Wilaya ya Geita na kuzikwa katika Kijiji cha Nakasenya, Kata ya
Butundwe, lakini juzi alfajiri alikutwa ameketi nje ya nyumba ya dada yake
aitwaye Monica James, anayeishi Kasamwa.
Aliyekuwa wa kwanza kumwona Flora ni mdogo wake aitwaye Monica Onesmo
ambaye baada ya kuamka saa 11:00 alfajiri nyumbani kwa dada yake, alimwona
mwanamke aliyekuwa ameketi nje ya nyumba hiyo, lakini alimfananisha mwanamama
huyo na marehemu dada yake.
“Baada ya kumwona nilimwita mtoto wake tunayekaa naye na nikampigia
simu dada (Monica) ambaye alikuwa amelala chumba kingine nikamwambia kwamba
nimeamka na kumkuta mwanamke amekaa hapa nje, lakini kila nikimwangalia
anafanana na marehemu dada yetu,”alisema Jubili na kuongeza kwamba alipowaita
wote walitoka nje.
Alisema mtoto wa Flora (marehemu anayedaiwa kufufuka) anaitwa Rebeka
Elisha (16) na kwamba walimchukua tangu 2008 wakati mama yake huyo alipofariki
dunia katika Hospitali ya Geita ambako alikuwa amelazwa kutokana na kusumbuliwa
na ugonjwa wa ini.
Rebeka ambaye ni mtoto wa nne wa Flora alisema: “Mama mdogo alituita
sisi tulikuwa tumelala akasema kwamba nje kuna mwanamke ambaye anafanana na
marehemu mama yetu, ndipo na sisi tukatoka na kweli kumwangalia alikuwa ni yeye
kabisa.”
Alisema walipomuhoji mama yake huyo kwamba ametokea wapi, aliwaeleza
kuwa ametoka eneo la Katoro kwa mganga na aliletwa na watu ambao hakuwatambua
Alhamisi saa 1:30 usiku ndani ya gari na watu hao walimshusha kwa mtu aitwaye
Juma Luchunga ambaye ni jirani na dada zake hao.
Kauli ya Flora
Akizungumza na waandishi wa habari, Flora alisema yeye ni mkazi wa
Katoro na kwamba alitokea Katoro nyumbani kwa mganga wa jadi ambaye hata hivyo
hakumtaja kwa maelezo kwamba wataalamu wake (majini) wamemkataza.
“Nilikuwa naishi kwa mganga wa kienyeji ila alikuja mwanaume wakati
nikiwa pale akaninywesha dawa kisha tukapakizwa kwenye gari na watu wawili
ambao sikuwatambua, mmoja mwanamke na mwingine mwanaume mpaka hapa Kasamwa
tukashushwa saa 1:00 jioni,”alisema Flora.
Alisema alipofika Kasamwa alikwenda kunywa uji kwa mama mmoja ambaye
pia hakumtaja na kwamba baadaye alipelekwa nyumbani kwa mtu mwingine saa nne
usiku, lakini watu wa nyumba hiyo walipomwona walimwambia: “Hapa si kwako
twende tukupeleke kwa ndugu yako” na ndipo wakampeleka kwa dada yake ambako
aliketi nje hadi alfajiri.
Flora alisema kabla ya kuishi kwa mganga alikuwa akiishi porini ambako
alitupwa na watu asiowafahamu na baadaye aliokotwa na wasamaria wema ambao
ndiyo walimpeleka kwa mganga ambako alikuwa akiishi muda wote.
No comments:
Post a Comment