Waasi wa
kundi la M23 wameitaka Tanzania kuachana na mipango ya kuchangia wanajeshi wake
katika kikosi cha Umoja wa Mataifa kinachopangwa kutumwa mashariki mwa Jamhuri
ya Kidemokrasi ya Congo kupambana na waasi .
Waasi wa kundi hilo la M23 ambao wamekanusha madai ya wataalamu wa
Umoja wa Mataifa kwamba nchi jirani za Rwanda na Uganda zinawaunga
mkono,wameonya katika baruwa iliyotumwa na kiongozi wa kisiasa wa kundi hilo
Betrand Bisimwa kwa Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania kwamba daima wamekuwa
wakipata ushindi dhidi ya vikosi vikubwa vyenye silaha nzuri.
Bisimwa ameandika " Jambo kama hilo litawakuta kikosi hicho cha
Umoja wa Mataifa cha kuingilia kati iwapo busara yao itashindwa kufanya kazi
kuingilia kati na kuzuwiya hali ya hatari ilioko kwenye mkondo huo."
Bisimwa amesema kwa ajili hiyo kundi hilo la waasi la M23 linaomba
bunge na wananchi wa Tanzania kufikiria upya kwa uangalifu juu ya hali hiyo na
kuishawishi serikali ya Tanzania kutowapeleka watoto wao wa kiume na wa kike wa
taifa hilo la uadilifu kushiriki kwenye vita vya kipuuzi dhidi ya ndugu zao wa
Congo.
M23 kujibu mapigo ikishambuliwa
Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania.
Hapo Ijumaa kundi hilo lilionya kwamba watalipiza iwapo watashambuliwa
na kikosi cha kuingilia kati mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
ambacho kitakuwa sehemu ya Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kuleta Utulivu
kikiwa na jukumu la kuwalinda raia.
Msemaji wa kundi hilo la waasi Vianney Kazarama aliliambia shirika la
habari la AFP kwamba wao kundi la M23 hawana haki ya kushambulia kikosi cha
Umoja wa Mataifa lakini iwapo kikosi hicho kitawashambulia wana haki ya
kuchukuwa hatua ambapo watalipiza na watajihami.
Hapo tarehe 28 mwezi wa Machi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa
kauli moja limeidhinisha kuundwa kwa kikosi cha zaidi ya wanajeshi 2,500 kikiwa
na mamlaka ya kufanya mashambulizi ya kuwalenga waasi mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo eneo lenye utajiri wa madini ambalo limekumbwa na mzozo
kwa zaidi ya miongo miwili.
Ni tangazo la vita
Waasi wa M23 wakiweka ulinzi wakati wa kuchaguliwa kwa Bisimwa kuwa
kiongozi wa kisiasa wa kundi hilo mwezi wa Machi 2013
Siku chache baada ya kupitishwa kwa uamuzi huo wa Umoja wa Mataifa
kiongozi wa kisiasa wa kundi la M23 Bertrand Bisimwa aliita hatua hiyo kuwa ni
tangazo la vita wakati mazungumzo ya kutafuta amani kati ya kundi hilo na
serikali yakiwa yanaendelea mjini Kampala Uganda. Madnodie Muonoubai msemaji wa
Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kuleta Utulivu ambacho kitajumuisha kikosi
kitakachotumwa Congo amesema idadi rasmi ya wanajeshi watakaounda kikosi hicho
ni 3,069.
Afrika Kusini,Tanzania na Malawi vitachangia wanajeshi wao katika
kikosi hicho ambapo kila nchi itatuma wanajeshi 850 wa nchi kavu na kufikisha
jumla ya wanajeshi 2,550. Msemaji huyo ameongeza kusema kwamba wanajeshi
waliobakia 519 watatawanya katika vikosi vya mizinga, vikosi maalum na vikosi
vya upelelezi.Kikosi hicho kitaongozwa na generali wa Tanzania.
Afrika Kusini na mdahalo wa kutuma wanajeshi
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini akihutubia wakati wa misa ya
kumbukumbu ya wanajeshi wake waliouwawa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Suala la kutumwa kwa wanajeshi wa Afrika Kusini nchi za nje limezusha
mjadala nchini humo kufuatia kuuwawa kwa wanajeshi wake 13 katika Jamhuri ya
Afrika ya Kati mwishoni mwa mwezi uliopita wakati waasi walipompinduwa Rais
Francois Bozize.
Kundi la waasi wa M23 tayari limelitaka bunge la Afrika Kusini katika
baruwa yao ya tarehe 3 Aprili kutochangia wanajeshi wake katika kikosi cha
Umoja wa Mataifa kitakachotumwa Congo. Msemaji wa jeshi la Afrika Kusini
Brigedia Generali Xolani Mabanga ameliambia shirika la habari la AFP kwamba
wanavizingatia vitisho vinavyotolewa na kundi la waasi la M23 lakini wao sio wa
kuamuwa iwapo wapeleke au wasipeleke wanajeshi hao na kwamba watapeleka
wanajeshi watakapoagizwa na serikali lakini hakuna kitakachowarudisha nyuma au
kuwafanya wahofu.
Amesema "Iwapo tutaweka wanajeshi Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
kama sehemu ya kikosi cha Umoja wa Mataifa,tutafanya hivyo. Mojawapo ya
majukumu yetu ni kwenda vitani,kupigana vita na kushinda vita." Kundi la
M23 lililopewa jina kutokana na makubaliano yake ya amani na serikali
yaliosainiwa tarehe 23 mwezi wa Machi mwaka 2009, limeibuka kutokana na uasi
jeshini wa jamii ya Watutsi hapo mwezi wa Aprili mwaka 2012 kwa misingi kwamba
serikali haitekelezi makubaliano hayo.
Walinda amani na mamlaka ya kushambulia
Waasi wa M23 wakati walipouteka mji wa Goma.
Waasi hao waliuteka kwa muda mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini wa
Goma mwezi wa Novemba mwaka jana. Waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo Raymond Tshibanda amesema kikosi hicho cha Umoja wa
Mataifa cha kuingilia kati mashariki mwa Congo kitawekwa kufikia mwishoni mwa
mwezi wa Aprili lakini wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanataraji kwamba
itachukuwa wiki kadhaa kabla ya kuanza kufanya kazi.
Hii ni mara ya kwanza kwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa
kupatiwa mamlaka ya kufanya mashambulizi.
No comments:
Post a Comment