Language

Thursday 28 February 2013

HABARI MUHIMU: TABIBU ALIYEMTOA MIMBA BAAMEDI KUPANDISHWA KIZIMBANI

POLISI Bunda wamesema watamfikisha mahakamani wakati wowote Ofisa tabibu mmoja wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, anayetuhumiwa kumtoa mimba mhudumu mmoja wa baa ambaye kwa sasa hali yake ni mbaya.

Ofisa tabibu huyo Michael Musimu, ambaye amekuwa akifanya kazi katika kituo cha afya Manyamanya, kilichoko Bunda, anashikiliwa na polisi akituhumiwa kumtoa mimba  mhudumu mmoja wa baa ijulikanayo kwa jina la Savana, iliyoko mjini hapa.
Polisi wamemtaja mhudumu huyo kuwa ni Salome Saimon Bugunda, ambaye sasa hali yake ni mbaya na amepelekwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando Mwanza kwa matibabu zaidi.
Imedaiwa kuwa tukio hilo lilitokea juzi na kwamba baada ya Musimu kumtoa mimba mhudumu huyo, hali yake ilibadilika na kumpeleka katika kituo cha afya Manyamanya, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya zaidi na ndipo akakimbizwa katika hospitali ya DDH Bunda ambako pia alipewa rufaa ya kwenda Bugando.
Aidha, imeelezwa kuwa mhudumu huyo ameumizwa vibaya kwani sehemu ya utumbo wake umetoka nje.
Kukamatwa kwa ofisa tabibu huyo kumetokana na mwanamke huyo kumtaja bayana kwa kuwaambia ndugu zake ambao walitoa taarifa polisi. Licha ya polisi kuthibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kumshikilia mtuhumiwa huyo, lakini Kamanda wa Polisi Mara, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Absalum Mwakyoma amesema bado hajapatiwa taarifa kamili juu ya tukio hilo na kuahidi kulifuatilia.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...