Language

Monday 4 March 2013

HABARI MUHIMU: UNAIKUMBUKA STORI YA JANA KUHUSU KIFO CHA MJUMBE WA UVCCM BESON MOLLEL? MUENDELEZO WAKE HUU HAPA BAADA YA UCHUNGUZI

UCHUNGUZI wa awali wa kifo cha aliyekuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), kupitia Mkoa wa Arusha, Benson Mollel (26) umeonyesha kuwa chumbani alimofariki kulikutwa mipira miwili ya kiume, mmoja ukiwa umetumika.

Marehemu Mollel alikutwa amekufa juzi ndani ya Hoteli ya Lush Garden Business, Mtaa wa Jacaranda, Arusha katika mazingira ya kutatanisha huku mwili wake ukiwa mtupu. Anatarajiwa kuzikwa kesho Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema pia kuwa ndani ya chumba alichofia, ilikutwa silaha aina ya bastola, kiasi kidogo cha madini ya Tanzanite, simu mbili, kadi za benki na fedha ambazo kiasi chake hakikutajwa.
“Kwa sasa bado tunachunguza tukio hilo kwa kuwa linatawaliwa na utata kwani marehemu hakukutwa na aina yoyote ya jeraha mwilini... uchunguzi wa kina utafanyika kubaini nini kilisababisha kifo cha Mollel kwa kushirikiana na familia yake.”
Kamanda Sabas alisema pia kuwa licha ya marehemu kujishughulisha na siasa pia alikuwa akifanya kazi katika Kampuni ya Madini ya Manga Germs iliyopo Arusha
Baadhi ya mashuhuda walisema, kabla ya marehemu kukutwa na mauti hayo, alitembelewa na wanawake wawili Jumamosi na Jumapili iliyopita, ndani ya chumba chake.
Mmoja wa mashuhuda hao, ambaye ni mhudumu wa hoteli alisema alimpokea mwanamke mmoja akimtaka Mollel, Jumapili iliyopita.
Mhudumu huyo (jina tunalo) alisema mwanamke huyo alionekana hotelini hapo kwa mara ya kwanza siku hiyo na mkononi alikuwa ameshikilia kipochi kidogo cha mkononi (wallet) na aliingia chumbani kwa marehemu na kutoka baada ya dakika 15.
“Alipofika hapa hotelini dada huyo aliomba tumpeleke chumba hicho namba 214 baada ya kuwasiliana na marehemu... tukamwelekeza akaenda lakini sura hii tulikuwa hatujawahi kuiona,” alisema.
Naye mlinzi wa hoteli hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Obeid Mollel kutoka Kampuni ya Ulinzi ya Victoria Support Services inayolinda hoteli hiyo, alisema alimwona dada huyo aliyekuwa na marehemu akitoka nje ya uzio wa hoteli akiwa hana kitu chochote mkononi na aliondoka kwa miguu bila usafiri wowote.
Mtumishi wa chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mount Meru, Francis Costa 'Rasta', alithibitisha kuona mipira hiyo ya kiume iliyokuwa imehifadhiwa katika shuka lililokuwa limehifadhi mwili wa marehemu ulipofikishwa hapo saa 8.30 usiku.
Alisema muda mfupi baada ya kuukabidhi mwili huo na kuondoka, maofisa wa polisi waliopeleka walirejea na kuchukua mipira hiyo.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru, Dk Frida Mokiti alisema utaratibu wa kuufanyia uchunguzi utategemea maagizo ya polisi.


No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...