Language

Monday 4 March 2013

HABARI TOKA KENYA: UHURU KENYATTA ANAONGOZA KATIKA UCHAGUZI, 22 TAYARI WAMEUAWA


Matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu nchini Kenya yanaonyesha kuwa Uhuru Kenyatta, mtoto wa Rais wa Kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta anaongoza, huku akifuatiwa kwa karibu na aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Raila Odinga.
Kama alivyo Uhuru, Raila pia ni mtoto wa mmoja wa waasisi wa taifa la Kenya, ambaye alikuwa Makamu wa Mzee Kenyatta, Jaramong Oginga Odinga.

Hadi majira haya ya  saa 6.45 usiku wa kuamkia leo,  Uhuru ambaye ni mgombea wa TNA alikuwa amepata kura 744,648 sawa na asilimia 56.1 wakati Raila ambaye ni mgombea wa ODM alikuwa akifuatia kwa kupata kura 527, 780 sawa na asilimia 39.7.
Matokeo hayo ni kutoka katika vituo zaidi ya 5000 kati ya 31,000 na yalikuwa yakionyeshwa moja kwa moja na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) kadri yalivyokuwa yanaingia.
Hata hivyo Mwenyekiti wa IEBC, Isaack Hassan akizungumza na vyombo vya habari jana usiku alisema matokeo hayo ni ya awali na kwamba matokeo kamili yangetangazwa na tume yake baada ya kukusanya taarifa kutoka vituo vyote vya kupigia kura.
Wagombea wengine walikuwa wameachwa mbali. Hao ni Musalia Mudavadi, Peter Kenneth, James Kiyiapi, Martha Karua, Mohamed Dida na  Paul Muite.
Waliokufa wafikia 22
Mapema watu 22 wakiwamo askari polisi tisa waliripotiwa kuuwawa  baada ya kuvamiwa na kikundi cha watu zaidi ya 200 huko Mombasa na Kilifi saa chache kabla ya Wakenya kuanza kupiga kura jana.
Saa chache kabla ya uchaguzi huo, askari polisi tisa waliuawa katika mashambulizi yaliyotokea kwenye miji ya Mombasa, Kilifi na Kwale na kuacha wavamizi wapatao 10 na raia wa kawaida watatu pia wakifariki.
Baada ya vifo hivyo, serikali ilipeleka vikosi vya askari kutoka Mariakani Barracks kwenda kutuliza ghasia hizo wakati kundi lingine la askari lilitoka Nyali Barracks kwa ajili ya kuweka doria katika miji ya Mombasa na North Coast.
Taarifa zilizopatikana baadaye jana zilisema kuwa kwenye mji wa Mombasa askari polisi wanne waliuawa na watu zaidi ya 100 waliovamia kituo cha kura cha Miritini.
Polisi pia ilithibitisha kuuawa kwa watu saba katika mapigano hayo huku na wengine kadhaa kutiwa nguvuni.
Wavamizi wengine waliuawa katika miji ya Kisauni na Kilifi huku polisi wanne wakiuawa Chumani na mmoja huko Chonyi huku watu watatu wakiuawa kwa kupigwa risasi.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...