Language

Tuesday 5 March 2013

MICHEZO: WACHEZAJI WA SIMBA WAMUANGUKIA KOCHA


BAADHI ya mastaa wa kikosi cha kwanza, Simba (majina tunayo) wamesema hawana imani na mbinu za Kocha Mkuu Patrick Liewig na hilo limethibitika zaidi katika mchezo wao wa Angola.

Mwishoni mwa wiki, Simba ilishambuliwa na kipigo cha mabao 4-0 kutoka  Recreativo Libolo ya Angola katika mchezo wa marudiano Ligi ya Mabingwa Afrika.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kuaga mashindano raundi ya kwanza kwa jumla ya mabao 5-1, kutokana na kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita, Dar es Salaam.
Wakizungumza juzi usiku kwenye hoteli ya Ritz iliyopo mji wa Calulu lilikofanyika pambano hilo la marudiano, mastaa hao wamesema mfumo wa sasa wa Simba ni kujihami zaidi kuliko kushambulia.
"Mbinu nyingi tunazotumia ni za kujihami. Mazoezini hatufundishwi kucheza soka la kushambulia na badala yake kocha amekuwa akitumia muda mwingi kutufundisha namna ya kukaba maadui katika maeneo yetu."alisema mchezaji mmoja nyota katika nafasi ya kiungo.
"Mimi siyo msemeji, lakini sasa hivi inabidi niseme. Wachezaji vilevile hatuko fiti. Tunafanya mazoezi kwa dakika chache, hatujawahi kucheza mazoezi ya mechi miongoni mwetu. Uimara wa timu unaanzia mazoezini na sisi hatuko imara." aliongeza staa huyo.
Nyota mwingine wa Simba anayecheza nafasi ya ushambuliaji alisema: "Kutokuwapo Emmanuel Okwi na Patrick Mafisango (marehemu), siyo sababu ya timu kufanya vibaya. Nadhani kocha (Liewig) abadili mbinu."
"Kuna mechi nyingi Okwi hakucheza na bado tulishinda. Mimi sifurahishwi na jinsi tunavyocheza kwa kumtegemea mshambuliaji mmoja mbele." alisema mshambuliaji huyo.
Nyota mwingine wa safu ya ulinzi alihoji mantiki ya viongozi na Benchi la Ufundi kumsajili kipa wakati wa dirisha dogo, huku timu ikiwa na upungufu wa wachezaji katika safu ya ushambuliaji.
Aidha, kiongozi wa msafara wa Simba na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Zacharia Hans Pope amekuja na hoja tofauti na malalamiko ya wachezaji dhidi ya kocha wao.
Hanspope amesema Simba imefungwa kwa sababu wapinzani wao Libolo walijiandaa vizuri kwa mazingira yote, ndani na nje ya uwanja kulinganisha na Simba.
"Yatasemwa mengi, lakini ukweli tumetolewa na timu yenye uwezo kuliko sisi. Wenzetu wamefanya maandalizi mazuri. Kumbuka kuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani waliwahi kuichapa Orlando Pirates ya Afrika Kusini 3-0." alisema Hans Pope.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...