Language

Friday, 8 March 2013

HABARI MUHIMU: DAWA ZA KUTULIZA MAUMIVU ZINAMADHARA MAKUBWA KIAFYA, SOMA HAPA

Dawa maarufu za maumivu zilizozagaa katika maduka ya dawa nchini zinatajwa kuchangia ugonjwa wa kiharusi, moyo, vidonda vya tumbo na vifo vya ghafla, imebainika.

Imeelezwa kuwa watu wanaotumia dawa za kutuliza maumivu za Ibuprofen, Diclofenac na Diclopar mara kwa mara wapo katika hatari ya kupata maradhi ya moyo na kiharusi kwa asilimia 40 na hufa vifo vya ghafla.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika Jiji la Dar es Salaam na viungo vyake umebaini kuwa madaktari wengi huwaandikia wagonjwa dawa hizo, zikiwa ndizo dawa maarufu za kutuliza maumivu.
Madaktari  na wafamasia hao waliulizwa kwa nyakati tofauti na Mwananchi, ni dawa zipi za maumivu wanazowaandikia mara kwa mara wagonjwa na wakazitaja kuwa ni Diclofenac, Ibuprofen, Diclopar, Paracetamol na  Tiroxam.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, kutoka Taasisi ya Moyo Tanzania, Ferdinand Masau anasema  kwa kawaida dawa zote zina madhara, ingawa hana uhakika iwapo dawa hizo zina athari kwenye moyo.
“Kwa ninavyojua dawa hizi zikitumiwa mara kwa mara zinasababisha michubuko tumboni na kusababisha vidonda vya tumbo,” anasema Dk Masau.
Mtaalamu wa Famasia ambaye hakupenda kutajwa jina lake alisema ana uhakika kuwa paracetamol (panadol) ikitumiwa kwa muda mrefu inaweza kusababisha matatizo katika ini na pia dawa hizo za maumivu huchochea vidonda vya tumbo.
“Paracetamol na Diclofenac zinaweza kusababisha ‘ulcers’ (vidonda vya tumbo) na baada ya muda mtu huweza kupata saratani ya ini, lakini kwa madhara mengine yaliyotajwa sina uhakika sana,” alisema famasia huyo.
Aidha, uchunguzi wa Mwananchi ulibaini kuwa wengi wanaotumia Diclofenac na Ibuprofen mioyo yao huwaenda mbio dakika chache baada ya kuzimeza.
Licha ya kuzungumza na madaktari, Mwananchi lilipita katika maduka kadhaa ya dawa na kugundua kuwa dawa hizo  huuzwa kwa wingi, tena bila ya cheti cha daktari.
Dawa  maarufu ya Ibuprofen inatajwa kuchangia kwa asilimia 18 shinikizo la damu na kiharusi.
Diclofenac inayopendelewa na watu wengi kwa kutuliza maumivu haraka  nayo imebainika kuchangia maradhi hayo kwa asilimia 51.
Kwingineko, utafiti uliofanywa katika nchi 51 duniani ikiwemo Tanzania umeonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 2.7 hufa kutokana na matumizi ya dawa hizi.
Dawa hizi aina ya NSAIDS kwa kawaida hutumika kutibu maumivu, uvimbe, maumivu ya mgongo, kichwa, homa, mafua na kushusha joto la mwili.
Takwimu zimeonyesha kuwa  matumizi ya dozi ndogo tu ya diclofenac hasa kwa  kutuliza maumivu kwa watu waliotoka kufanyiwa upasuaji  huchangia kwa asilimia 22  maradhi ya moyo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...