Mahakama ya Juu (Supreme Court) nchini Kenya jana ilitupilia mbali viapo
viwili katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Uhuru
Kenyatta wa Muungano wa Jubilee.
Maombi yaliyotupwa ni lile la muungano wa mashirika yasiyo ya
kiserikali lililoitaka mahakama iamuru tume ya uchaguzi kufikisha mahakamani
hapo nyaraka zote zilizotumika wakati wa uchaguzi huo.
Kadhalika mahakama hiyo ilitupilia mbali hati ya kiapo yenye kurasa 839
kilichowasilishwa na upande wa Muungano wa Cord ambacho kilidai kwamba kura
katika majimbo 120 zilikuwa haziwiani na idadi ya wapigakura, hivyo kuitaka
mahakama hiyo iitishe uchunguzi wa kina kwa daftari hilo pamoja na kura
zilizopigwa.
Katika kiapo cha Cord, Jaji Phillip Tunoi alisema kwa mujibu wa sheria
hati za kiapo si haki ya mlalamikaji au mlalamikiwa hivyo kabla wa kuwakilishwa
walalamikaji walipaswa kupata ruhusa ya mahakama, jambo ambalo halikufuatwa.
Kwa upande wake Jaji Mohammed Warsame aliyesoma uamuzi dhidi ya kiapo
cha mashirika yasiyokuwa ya kiserikali alitupilia mbali maombi yao kwa maelezo
kwamba yalifikishwa mahakamani nje ya muda uliowekwa kisheria.
Katika ombi lao muungano huo wa Africog ulidai kuwa kufeli kwa mfumo wa
kielectronikiwa kuhesabu kura ulikuwa umepangwa kwa madhumuni ya kuiba kura.
Hivyo tume hiyo iamuriwe kuleta mahakamani hapo nyaraka zote ili zifanyiwe
uchunguzi wa kitaalamu.
No comments:
Post a Comment