Shirika la kutetea haki za kibinadamu, Human Rights Watch, limesema kuwa
makundi yaliyojihami nchini Somalia ikiwemo majeshi ya serikali, yamefanya
vitendo vya ubakaji, kuwachapa na kuwadhulumu watu walioachwa bila makao au
wakimbizi.
Ripoti ya shirika hilo imegusia wale watu waliokimbia vita tangu mwaka
2011 kwa sababu ya njaa, na sasa wanaishi katika kambi mjini Mogadishu.
Katika ripoti hiyo mpya, shirika hilo limesema kuwa wasimamizi wa kambi
hizo , wanaojulikana kama walinzi, huiba msaada wa wakimbizi hao na hata
kuwadhulumu.
Shirika hilo linasema , kuwa wakimbizi wa ndani, hasa wanawake
wameripoti kubakwa na kudhulumiwa na watu waliovalia sare za kijeshi na wengine
wanaoaminiwa kuwa wapiganaji wa makundi ya waasi.
Linasema kuwa baadhi ya vitendo vibaya vya dhuluma walivyofanyiwa ni
pamoja na dhulma za kingono dhidi ya wanawake na wasichana.
Kadhalika ripoti hiyo imewanukuu wanawake wanaodai kubakwa akiwemo
mwanamke mwenye umri wa miaka
23 aitwaye, Quman.
23 aitwaye, Quman.
Anasema alikuwa na ujauzito wa miezi, tisa alipobakwa na kundi la watu
asiowajua ingawa walikuwa wamevalia magwanda ya kijeshi.
Mwanamke mwingine, Safiyo, alilazimika kukatwa mguu wake baada ya
kubakwa na kisha kupigwa risasi.
Aidha ripoti hiyo inasema kuwa visa vya ubakaji haviripotiwi sana kwa
sababu ya hofu ya wanawake kuwa watafanyiwa unyanyapaa na kutengwa na jamii.
''Uchunguzi wetu umeonyesha kuwa watu katika kambi hizo huwekwa kama
watumwa. Hawawezi kuondoka, walinzi wa kambi hizo wenyewe wanafanya dhulma. Wao
huiba msaada ambao hutolewa kwa wakimbizi. Watu wengi kwa sasa wanahitaji
msaada wa haraka,'' ilinukuu ripoti hiyo.
Human Rights Watch pia limefichua visa vya ubaguzi wa kikabila hasaa
kwa wale wanaotoka katika jamii fulani. Linasema kuwa watu wengi wamelalamika
kuhusu visa vya kukamatwa kiholela na hata kudhulumiwa. Licha ya serikali ya
mpya ya Somalia kupiga hatua bado inakabiliwa na changamoto nyingi.
No comments:
Post a Comment