Idadi ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya jengo lililoporomoka Dar
Es Salaam jana asubuhi inazidi kuongezeka na sasa takriban watu 18 wamethibitishwa
kufariki.
Kamimishna wa polisi Saidi Meck Sadick alisema watu 21 walinusurika
kifo, aliongeza kuwa wangali wanawatafuta manusura.
Ripoti za mapema zilisema kuwa watu 45 ikiwemo wafanyakazi wa mjengo na
watoto wa shule ya mafunzo ya dini ya kiisilamu bado hawajaptikana.
Mwandishi wa BBC Hassan Mhelela anasema kuwa jengo hilo limeharibiwa
vibaya sana na kuwa lilikuwa liwe jengo na ghorofa kumi na mbili lakini wajenzi
walikuwa wamejenga hadi ghorofa 16.
Mmoja wa walioshuhudia tukio hilo Nishit Surelia, aliambia BBC kuwa
"tulisikia sauti kubwa na kisha jengo likaporomoka. Kila mtu alianza
kukimbia wakifikiria kuwa lilikuwa tetemeko la ardhi . Vumbi lilikuwa
limetapakaa. Na hapo ndipo tulijua kilichokuwa kimetokea.''
Manusura waliokuwa wamenaswa chini ya vifusi, inasemekana walikuwa
wanawapigia simu majirani na jamaa zao kuwafahamisha hali yao
Aidha Rais Jakaya Kikwete alitembelea eneo la ajali.
Jengo hilo lilikuwa karibu na msikiti pamoja na eneo la makaazi ya watu
na nyumba zingine za kibiashara mjini Dar es Salaam.
Polisi wanasema kuwa wanawahoji watu wanne waliohusika na ujenzi wa
jengo hilo wakati kukiwa na jengo lengine karibu na lilie liliporomoka ambalo
pia walikuwa wanasimamia shughuli za ujenzi wake. Jengo hilo litavunjwa baadaye
leo.
Uchumi wa Tanzania unaokuwa kwa kasi umesababisha ujenzi wa kasi mjini
Dar es Salaam, katika miaka ya hivi karibuni sawa na ilivyo katika miji mingi
ya kiafrika.
Lakini duru zinasema kuwa kasi ya ujenzi na ukosefu wa usalama wakati
mwingine inaweka katika hatari maisha ya watu na majengo.
No comments:
Post a Comment