HISTORIA ya Tanzania haiwezi kukamilika bila kutaja jina la mtu maarufu
aliyebuni jina la Tanzania ambaye kwa bahati mbaya au kwa makusudi hakumbukwi
tena.
Tunaelezwa kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lakini nani kati
yetu amekuwa akijiuliza jina la Tanzania lilivyopatikana na nani hasa
alilibuni?
Wengi tunaambiwa kuwa jina la Tanzania lilipendekezwa na Watanganyika,
Wazanzibari na raia wengine wa nje lakini hawatajwi waziwazi na picha zao
tukaziona.
Inaaminika kuwa mtu aliyebuni jina la Tanzania ni MOHAMMED IQBAL DAR,
raia wa India ambaye alikuwa miongoni mwa watu walioshindana katika shindano la
kubuni jina la nchi mpya baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana.
Mohammed alizaliwa mkoani Tanga miaka ya 1944; baba mzazi wa Mohammed
alikuwa daktari huko mkoani Morogoro akiitwa Dk. T . A DAR aliyefika Tanganyika
kuanzia mwaka 1930.
Mohammed Iqbal Dar alipata elimu yake ya msingi mkoani Morogoro katika
Shule ya Msingi H. H D Agakhan ambayo kwa sasa ni mali ya serikali. Alijiunga
na Shule ya Sekondari Mzumbe alikosoma kidato cha kwanza hadi cha sita.










