Language

Thursday 2 May 2013

VIWANDA VINNE VIMEFUNGWA KILIMANJARO


VIWANDA vinne vya kutengeneza pombe, kusindika maziwa na machinjio mawili yamefungwa katika wilaya za Rombo, Mwanga na Siha mkoani Kilimanjaro kutokana na kushindwa kukidhi vigezo vya ubora vilivyoainishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA).

 Mkaguzi wa Chakula Kanda ya Kaskazini, Abdalah Mkanza alisema ufungaji huo umefanikiwa wakati idara ya ukaguzi ya kanda hiyo ilipofanya ukaguzi wa kushitukiza kwa kushirikiana na wakaguzi wengine kutoka Kanda ya Mashariki.
Alisema ukaguzi ulifanyika kwa viwanda vyote vikubwa na vidogo mkoani Kilimanjaro na machinjio yote za mjini na vijijini ambapo walibaini wananchi wapo hatarini kupata magonjwa kutokana na mazingira halisi ya uchinjajio wa wanyama na viwanda hivyo.
Mkaguzi huyo alisema zoezi la ukaguzi litafanyika kwa mara nyingine mkoani humo kwa lengo la kutazama iwapo maeneo waliyoyapa maelekezo yamefuata ama la, ili hatua nyingine ziweze kuchukuliwa iwapo itabainika wamepuuza.
Aliwataka wafanyabiashara na waagizaji wengine wa bidhaa kutoka nje ya nchi kuwasiliana na TFDA ili kujiridhisha kama wanavyoagiza au kutumia kwa ajili ya walaji vimethibitishwa na mamlaka hiyo.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliohojiwa kuhusiana na kufungwa kwa viwanda vya pombe, Johnson Swai na Habibu Juma walipongeza juhudi hizo lakini wakataka ukaguzi huo kufanyika kila baada ya miezi sita kwani wapo wanaofungua viwanda na kufunga mara wanaposikia wakaguzi wanapita.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...