Mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa manane yaliyoendelea zaidi
kiviwanda wameungana kuilaani Korea Kaskazini, na kuitaka nchi hiyo kukomesha
mara moja kutoa vitisho vya kivita
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Wester Welle, amesema
katika siku ya pili ya mkutano wa mawaziri hao unaoendelea jijini London,
Uingereza, kuwa mataifa yote ya G8 yanaaminini kuwa kuongezeka kwa matamshi
hayo ya kuchochea vita kutoka kwa Korea Kaskazini lazima kusitishwe.
"Suala la kwa nini matamshi hayo ya kuchochea vita yanaongezeka –
ingawa ni muhimu, lakini halina uzito mkubwa. Muhimu zaidi ni kwamba matamshi
hayo hayapelekei kuripuka kwa vita. Na ndio maana ni muhimu sasa kuona jumuiya
ya kimataifa ikiwajibika na kuzungumza kwa sauti moja.
Siyo pekee nchi za
magharibi zinazobidi kuwa na msimamo mmoja, bali pia China na Urusi. Maoni
yangu ni kwamba nchi hizi mbili pia zingependelea hivyo," alisema Wester
Welle.
Korea kaskazini imetoa vitisho dhidi ya Korea Kusini, Japan na Marekani
na inaonekana kujiandaa kufanya majaribio kadhaa ya makombora ambayo wadadisi
wanasema huenda ikayafanya kwa wakati mmoja. Waziri wa mambo ya kigeni wa
Uingereza, William Hague, alisema nchi iko njia panda hivi sasa, na inaweza
kuishia kuwa taifa lililosambaratika na kutengwa, iwapo itashindwa kushiriki
mazungumzo.
No comments:
Post a Comment