Wanawe rais mstaafu wa Afrika Kusini Nelson Mandela, wameamua kuchukua
hatua za kuwaondoa wasaidizi wake watatu kutoka katika makampuni anayoyamiliki.
Hii ni kwa mujibu wa vyombo ya habari nchini humo.
Makaziwe na Zenani Mandela wanadai kuwa watatu hao hawana haki ya kuwa
kwenye bodi mbili za kampuni hiyo ambazo ni za thamani ya dola milioni 1.1
Mmoja wa wasaidizi hao, ambaye pia ni wakili wa Mandela, George
Bizos,amekana madai hayo.
Kesi hiyo inakuja wakati kuna wasiwasi mkubwa kuhusu afya ya Mandela
mwenye umri wa miaka 94
Mandela aliondoka hospitalini baada ya kutibiwa ugonjwa wa mapafu
pamoja na homa ya mapafu.
Mandela alilazwa hospitalini mara ya nne katika kipindi cha miaka
miwili.
Duru zinasema kuwa kumekuwa na mzozo wa kichinichini tangu mwaka 2005
wa kudhibiti pesa zinazotokana na mauzo kwenye jina la Mandela hususan picha
alizokuwa anachora akiwa jela.
Makaziwe na Zenani Mandela waliwasilisha kesi mahakamani wakidai kuwa
bwana Bizo, waziri wa nyumba, bwana Tokyo Sexwale na wakili wa zamani wa
Mandela, Bally Chuene, hawakuwahi kuteuliwa kama wamiliki au wakurugenzi wa
kampuni ya Harmonieux Investment Holdings na Magnifique Investment Holdings,
kulingana na gazeti la Star.
Pesa zinazotokana na makampuni hayo zinapaswa kuwafaidi wanawe Mandela
na yeye mwenyewe.
"Bizos, Chuene na Sexwale hawakuwahi kuteuliwa rasmi kama washika
dau katika kampuni hiyo.''
Bwana Bizos, wakili anayeheshimika sana na ambaye pia ni rafiki wa
karibu sana wa bwana Mandela, alisema kuwa watajitetea vikali katika kesi hiyo.
Aliongeza kuwa wanawe Mandela walikuwa wanataka kuuza vitu ambavyo
havipaswi kuuzwa .
No comments:
Post a Comment