Mama wa marehemu Kanumba Flora Mtegoa amesema anampenda msanii Elizabeth
Michael maarufu kwa jina la Lulu, licha ya matatizo yote yaliyotokea na kwamba
anamwachia Mungu katika yote.
Akizungumza na Mwananchi katika makaburi ya Kinondoni mara baada
ya misa maalum ya kumuombea marehemu na kuweka mashada ya maua Mtegoa alisema
yeye ni mkristo hivyo hana kinyongo na mwigizaji huyo.
"Mimi ni mkristo tumeambiwa samehe mara saba sabini, binafsi
sina kinyongo chochote na ninampenda kama ilivyokuwa kwa mwanangu, ila kila
ninapomuona siachi kumkumbuka mwanangu," alisema Mtegoa.
Alisema Kanumba alikuwa ni kama mtoto, mume, kaka na kama rafiki
yake, alimfanya kuwa mtu wa karibu yake na anashukuru mwanaye pia alimfanya
ajisikie furaha muda wote.

Akizungumzia suala ya ushiriki wake katika filamu ya Without
Daddy Mtegoa alisema "Nilikuwa naigiza tangu nasoma sekondari lakini sanaa
hapo nyuma haikulipa hivyo sikuendelea na sanaa, baada ya kufariki Kanumba
niliombwa nicheze filamu ya Without Daddy, nilikubali na ikawa filamu yangu ya
kwanza," alisema.
Alisema kwa sasa yeye anafanya kazi chini ya Kampuni ya Kanumba
The Great, hivyo itakapotokea filamu nyingine yupo tayari kuicheza.
No comments:
Post a Comment