Language

Friday 25 January 2013

HABARI: KESI YA SISTA ALIYEFUMANIWA NA MUME WA MTU SUMBAWANGA KUSIKILIZWA TAREHE 29

KESI  ya  madai  inayomkabili aliyekuwa  Mtawa wa Shirika la Kitawa la Kanisa Katoliki Jimbo la Sumbawanga, Sista Yasinta Sindani anayedaiwa kufumaniwa na mume wa mtu imepangwa  kusikilizwa Januari 29 mwaka huu.
“Sista’ Yasita  licha ya kuwa mtumishi  wa afya katika  Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini hapa  lakini inadaiwa  ameachana  na maisha  ya  kitawa  miaka  miwili  iliyopita kwa hiyari yake akiwa Mtawa  wa Shirika la  Masista wa Maria Mtakatifu Malkia wa Afrika (MMMA).
Shauri  hilo  la madai  linatarajiwa  kuanza kusikiliza  katika Mahakama ya Mwanzo mjini hapa, mbele ya Hakimu  Jaffari  Mkinga, mlalamikaji Asteria Mgabo anamtaka Yasinta amlipe Sh3 milioni baada ya kumfumania na mumewe wa ndoa aitwaye  Martin Msangawale (39), Mhasibu wa Manispaa ya  Sumbawanga.
Siku hiyo  ya kusikilizwa kwa shauri  hilo  mlalamikaji  katika  shauri  hilo  Asteria  anatarajiwa  kuwaleta  mashahidi wake  wanne mahakamani hapo
.
Katika hati ya  awali  ya madai inadaiwa kuwa mshtakiwa alifumaniwa na Asteria akiwa na mumewe  Msangawale wakiwa kwenye nyumba ya kulala wageni ya Chipu iliyoko eneo la Katandala mjini Sumbawanga usiku wa  Desemba 24 mwaka  jana siku ya mkesha wa  Sikukuu  ya Krismasi. Hakimu, Mkinga  alisema kuwa  kesi hiyo iliyokuwa isikilizwe Januari 21 imeahirishwa hadi  Januari 29 mwaka huu ili kumapatia  mlalamikaji muda wa  kuwaleta  mashahidi wake mahakamani.
Mlalamikaji  wa shauri  hilo la madai, Asteria  amedai  nje  ya mahakama kuwa alifunga ndoa  ya Kikristu  na mumewe  huyo Martin Msangawale  mwaka 2007.
Kesi hiyo inatarajiwa kuvuta hisia za watu wengi hususani wakazi wa Manispaa ya Sumbawanga na vitongoji vyake kutokana na kuwa gumzo kubwa na kuteka hisia za watu wengi hivi sasa.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...