Language

Saturday 13 April 2013

UMEME WAKATIKA NUSU SAA BAADA YA MITAMBO KUZINDULIWA ZANZIBAR



Huduma za umeme katika Mji wa Zanzibar, jana zilikatika kwa zaidi ya nusu saa baada ya kuzinduliwa kwa mradi mkubwa wa umeme  kutoka Tanzania Bara.

Uzinduzi wa mradi huo, ulifanywa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, katika  Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.
Sherehe za uzinduzi wa mradi huo, zilihudhuriwa pia na wananchi wa maeneo mbalimbali ya Zanzibar.
Hata hivyo muda mfupi baada ya shughuli hizo, huduma za umeme katika Mji wa Zanzibar, zilikatika  kuanzia saa 9 mchana na kudumu kwa zaidi ya nusu saa.
Meneja wa Shirika la Umeme la Zanzibar (Zeco), Mbarouk Hassan, alithibitisha kuwa huduma zilikatika na kwamba tatizo lilikuwa  Tanzania Bara.

“Umeme ulikatika kabisa, lakini tatizo lilianzia Bara,  hata hivyo limemalizika,” alisema Meneja huyo kwa njia ya simu.
Akizindua mradi huo uliogharimu Dola za Marekani 64.4 milioni Dk Shein aliwataka wananchi kulinda miondumbinu ya umeme kwa kuzingatia kuwa inatengenezwa kwa gharama kubwa.
Dk Shein ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, aliita Zeco kufuatilia madeni yake na kuwataka wananchi kulipia ankara za umeme.
Alisema kufanya hivyo kuatoa fursa nzuri kwa wawekezaji kuwekeza visiwani Zanzibar kwa sababu watakuwa na umeme wa uhakika.
Mradi huo unaotekelezwa kwa msaada wa Marekani,  umeanzia Ras Kiromoni wilayani  Bagamoyo hadi Mtoni Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...