Language

Friday 1 March 2013

HABARI MUHIMU: CHADEMA"HATUWATAKI WAZIRI WA ELIMU NA NAIBU WAKE"

WAKATI Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameunda tume kuchunguza matokeo mabaya ya mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012, Chadema kimesisitiza msimamo wake kwamba kitafanya maandamano kushinikiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Philipo Mulugo wajiuzulu.


Mapema wiki iliyopita Pinda alitangaza kuunda tume kuchunguza matokeo hayo, hatua ambayo Rais Jakaya Kikwete alitangaza kuiunga mkono katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi aliyoitoa juzi.
Lakini jana Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema watafanya maandamano makubwa aliyoyaita ya kihistoria, katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya na Dar es Salaam ili kushinikiza kutekelezwa kwa hatua hiyo.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Msakila, Sumbawanga mkoani Rukwa, Mbowe alisema: “Lengo la maandamano ni kuwataka waziri wa elimu na naibu wake wajiuzulu kwani wameshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kusababisha watoto wa maskini kufanya vibaya kwenye mitihani yao.”
Alisema maandamano hayo yatahusisha wafanyakazi wa Serikali, mama lishe na wafanyabiashara wa usafirishaji wanafunzi wa shule za msingi na sekondari... “Siku hiyo hakutakuwa na masomo wala kazi, kila kitu kitasitishwa.”
Mbowe alisema maandamano hayo yatakuwa ya kihistoria na kwamba Chadema kinataka kuwafungua macho wananchi walio na kipato cha chini ambao hawana uwezo wa kusomesha watoto wao nje ya nchi ili washinikize Dk Kawambwa na Mulugo waachie ngazi.
“Tunataka shule za sekondari na msingi zisigeuzwe kuwa vituo vya kulelea watoto, bali vifanye kazi za kutoa elimu, kama ilivyokusudiwa,” alisema Mbowe.
Hata hivyo, Mbowe aliwataka wananchi kuwa makini na uchochezi unaofanywa na baadhi ya vyama vya siasa, badala yake waangalie chama chenye sera, mtazamo na harakati za kuleta mabadiliko yatakayokuwa na manufaa kwa Watanzania wote.
“Njia sahihi ni kuhakikisha mnajiondoa, kwani ili muweze kujua mustakabali wa maisha yenu ni lazima mhakikishe mnakuwa makini kufanya uamuzi ulio sahihi kwa viongozi mnaowataka, ”alisema Mbowe.
Hii ni mara ya pili katika mwaka huu kwa Chadema kutaka viongozi wajiuzulu. Mwezi uliopita, chama hicho kilimtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai wajiuzulu kwa maelezo kuwa wamekuwa wakiminya demokrasia, kuubana upinzani na kupendelea chama tawala (CCM) bungeni.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...