Language

Thursday 28 March 2013

KAMA UMESIKIA SAKATA LA MARINGO SABA KUNYWA SUMU BAADA YA KUMFUMANIA MKEWE, MKASA WOTE UPO HAPA


MCHEKESHAJI wa Kundi la Mizegwe, Rashid Coster ‘Maringo Saba,’ anadaiwa kumfumania mkewe anayefahamika kwa jina la mama Zai kisha kuamua kunywa sumu ikisemekana kuwa alitaka kujiua kwa hasira.

Chanzo makini kilichoomba hifadhi ya jina kimenyetisha kuwa, Maringo Saba aliandaa mtego wa fumanizi baada ya kuhisi mkewe anamsaliti kwa rafiki yake anayefahamika kwa jina moja la Sam.
Chanzo hicho kilizidi kushuka na mistari kwamba, baada ya staa huyo kuandaa mtego, ulizaa matunda Jumatano ya Machi 20, mwaka huu ambapo alimfumania mkewe akijivinjari na jamaa.
Sosi huyo alizidi kubainisha kuwa, mke wa Maringo Saba alipoona mumewe amemjazia umati kwa fumanizi hilo, alitimua mbio kwa vile ilidaiwa Maringo Saba alitishia kumfanyia kitu mbaya.
“Ilikuwa vurumai, watu waliokusanyika kufanya fumanizi walimtembezea kichapo Sam kabla hajafanikiwa kuchoropoka kwenye himaya ya chumba hicho na kujisalimisha katika Kituo cha Polisi Mwananyamala CCM,” kilisema chanzo.
Chanzo kingine kilicho karibu na mchekeshaji  huyo (jina lipo) kilidai kuwa, baada ya tukio hilo, Maringo Saba alikutwa chumbani kwake amezidiwa ndipo ndugu zake walipomkimbiza kwenye Hospitali ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa za madaktari, imedaiwa kuwa staa huyo alikutwa na kiasi kikubwa cha sumu mwilini ambayo haikujulikana mara moja ni ya aina gani.
Mara baada ya taarifa hizo kutua kwenye dawati la Amani, waandishi wetu walifika Hospitali ya Mwananyamala na kumkuta mchekeshaji huyo akiwa amewekewa dripu za dawa huku ndugu zake wakisema jamaa alichanganya pombe na dawa na siyo sumu kama ilivyodaiwa.
“Ndugu yetu hakunywa sumu, alichanganya dozi ya malaria na pombe ndiyo maana alizidiwa ghafla,” alisema mmoja wa ndugu hao aliyejitambulisha kwa jina la Rashid Khalfan.
Hata hivyo, maelezo ya Rashid yalipingana na ya baadhi ya wauguzi wa hospitali hiyo ambao kwa sharti la kutoandikwa majina yao gazetini walikiri msanii huyo kukutwa na sumu mwilini.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwinjuma, Allen Mwakitalima alikiri kuwepo kwa fumanizi, lakini kuhusu kunywa sumu alisema alisikia kwa watu mtaani ingawa kwake hajafikishiwa taarifa rasmi.
“Habari za fumanizi kwa Maringo Saba lilifika kwangu kiofisi, hata polisi walishakuja kuniulizia, ila kuhusu kunywa sumu nilisikia kwa watu mtaani, lakini sijapata taarifa rasmi kutoka kwa mjumbe wake, kwa hiyo likinifikia nitalishughulikia kiofisi,” alisema mwenyekiti huyo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...