HATIMAYE ujenzi wa kiwanda cha
kusafisha gesi kabla ya kusafirishwa kwenda Dar es Salaam umeanza mkoani
Mtwara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati
na Madini, Eliakim Maswi alisema jana kuwa ujenzi huo unaofanywa na Kampuni ya
China Petroleum and Technology Development Co-operation (CPTDC), ambao awali,
ulipaswa kuanza wiki iliyopita, umeanza juzi baada ya Serikali kufikia mwafaka na
wananchi wa Kijiji cha Msimbati kinapojengwa.
“Mkuu wa Wilaya ya Mtwara (Wilman
Ndile) na vijana wake walilazimika kufika Kijiji cha Msimbati, ambako wananchi
walikuwa na mgogoro na watu wa Marine Park,” alisema Maswi.
Alisema baada ya ziara hiyo
kushindwa kufanyika Jumapili iliyopita, uongozi wa wilaya ulikutana na viongozi
wa kijiji na kufikia mwafaka uliofanikisha kuanza kwa ujenzi huo.
Alisema kuanzia mradi huo kutatoa
ajira za kawaida kwa wakazi saba wa maeneo yanayozunguka mradi huo na kwamba
kazi hiyo itaongeza mahitaji ya bidhaa mbalimbali na huduma katika Kata ya
Msimbati
“Mathalan kuku, matunda na mboga
za majani vinahitajika sana. Sasa wananchi ambao awali, hawakutaka kuelezwa
lolote, wameanza kuchangamkia fursa hizo jambo ambalo litawanufaisha zaidi,”
alisema.
Ujenzi huo ulielezwa kuwa
unatekelezwa sambamba na mwekezaji kujenga visima vitatu vya maji safi na
salama kijijini Madimba.
Alisema mwekezaji pia atasambaza
umeme kwa kaya 300 za ndani na jirani ya kijiji hicho na kwamba vifaa
vitakavyotumika katika kazi hiyo vinatarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwezi huu.
Maswi alisema shule zote kwenye
Kata ya Msimbati kikiwamo Kijiji cha Madimba, zitakarabatiwa na mwekezaji huyo
ikiwa ni sehemu ya mpango wa wananchi waishio maeneo ya mradi kunufaika na uwekezaji.
Hata hivyo, habari nyingine
zinaeleza kuwa ulinzi umeimarishwa katika eneo hilo la mradi ili kuhakikisha
hali ya usalama inaendelea kuwapo.
No comments:
Post a Comment