WAKATI Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda ameunda tume kuchunguza matokeo mabaya ya mtihani wa Kidato cha Nne mwaka
2012, Chadema kimesisitiza msimamo wake kwamba kitafanya maandamano kushinikiza
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa na Naibu wake,
Philipo Mulugo wajiuzulu.
Mapema
wiki iliyopita Pinda alitangaza kuunda tume kuchunguza matokeo hayo, hatua
ambayo Rais Jakaya Kikwete alitangaza kuiunga mkono katika hotuba yake ya
mwisho wa mwezi aliyoitoa juzi.
Lakini
jana Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema watafanya maandamano makubwa
aliyoyaita ya kihistoria, katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya na Dar es
Salaam ili kushinikiza kutekelezwa kwa hatua hiyo.
Akizungumza
kwenye mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Msakila,
Sumbawanga mkoani Rukwa, Mbowe alisema: “Lengo la maandamano ni kuwataka waziri
wa elimu na naibu wake wajiuzulu kwani wameshindwa kutekeleza majukumu yao
ipasavyo na kusababisha watoto wa maskini kufanya vibaya kwenye mitihani yao.”
Alisema
maandamano hayo yatahusisha wafanyakazi wa Serikali, mama lishe na
wafanyabiashara wa usafirishaji wanafunzi wa shule za msingi na sekondari...
“Siku hiyo hakutakuwa na masomo wala kazi, kila kitu kitasitishwa.”
Mbowe
alisema maandamano hayo yatakuwa ya kihistoria na kwamba Chadema kinataka
kuwafungua macho wananchi walio na kipato cha chini ambao hawana uwezo wa kusomesha
watoto wao nje ya nchi ili washinikize Dk Kawambwa na Mulugo waachie ngazi.
“Tunataka
shule za sekondari na msingi zisigeuzwe kuwa vituo vya kulelea watoto, bali
vifanye kazi za kutoa elimu, kama ilivyokusudiwa,” alisema Mbowe.
Hata
hivyo, Mbowe aliwataka wananchi kuwa makini na uchochezi unaofanywa na baadhi
ya vyama vya siasa, badala yake waangalie chama chenye sera, mtazamo na
harakati za kuleta mabadiliko yatakayokuwa na manufaa kwa Watanzania wote.
“Njia
sahihi ni kuhakikisha mnajiondoa, kwani ili muweze kujua mustakabali wa maisha
yenu ni lazima mhakikishe mnakuwa makini kufanya uamuzi ulio sahihi kwa
viongozi mnaowataka, ”alisema Mbowe.
Hii ni
mara ya pili katika mwaka huu kwa Chadema kutaka viongozi wajiuzulu. Mwezi
uliopita, chama hicho kilimtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job
Ndugai wajiuzulu kwa maelezo kuwa wamekuwa wakiminya demokrasia, kuubana
upinzani na kupendelea chama tawala (CCM) bungeni.
No comments:
Post a Comment